SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa siku 14 kwa wadaiwa sugu wote linalowadai kulipa madeni yao, vinginevyo litawakatia huduma ya umeme. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk Tito Mwinuka alisema shirika hilo linadai jumla ya Sh bilioni 275.38. Alitaja makundi yanayodaiwa na shirika hilo kuwa ni wizara na taasisi za Serikali, zinazodaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linalodaiwa zaidi ya Sh bilioni 127.87 na kampuni binafsi na wateja wadogo, ambao deni lao ni zaidi ya Sh bilioni 94.97. “Pamoja na siku hizo 14, pia tutawapa notisi wadaiwa wote na kuwaarifu juu ya muda tuliowapa wawe wamekamilisha kulipa madeni yao, baada ya hapo shirika litachukua hatua ya kusitisha huduma ya umeme kwa wateja watakaoshindwa kuanza kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria,” alisisitiza Dk Mwinuka. Alisema wale wateja wadogo, Tanesco haitowaandikia kutokana na sababu ya wingi...