USHIRIKIANO NA MUONGOZO KATIKA JAMII YA KISLAAM

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Faidika na Hadithi. Katika kipindi chetu kilivyopita tulinukuu baadhi ya hadithi zinazohusiana na haya na staha kwa wanawake
katika jamii. Kipindi chetu cha wiki hii kitazungumzia mfano mwingine lakini mara hii ukiwa ni mfano wa kimaanawi wa kuwasaidia watu wengine ambao ni kumpatia mtu mwongozo na kumuongoza na kumnasihi. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Wakati mwanadamu anapokuwa anatangatanga katika jangwa na korongo la upotofu, hughafilika na Muumba wa ulimwengu huu, imani juu ya Allah pamoja na taklifu na majukumu ya kidini ambayo ni wajibu kwake kuyatekeleza. Endapo hali hii ya kutangatanga na kutojua la kufanya itaendelea, basi dhihirisho la ujahili na shaka humuandama mwanadamu huyu na hivyo kumuweka mbali na njia ya ukweli na haki. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 32 ya Surat al-Maida:
"Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote."
Katika kufasiri aya hii Imam Swadiq (as) anasema: "Endapo mtu atamuongoza mtu kuelekea upande wa uongofu basi ni kama vile amewaokoa watu wote na kila mtu ambaye atampeleka mtu upande wa upotofu basi ni kama vile amewaua watu wote."
Licha ya kuwa mafuhumu na maana ya kidhahiri ya aya hiyo ni umauti na uhai wa kimaada, lakini muhimu zaidi ya hilo ni maisha na kifo cha kimaanawi. Uokozi kutokana na upotofu na ujahili ndio ile hali ya kumpa uhai mtu. Na kumpoteza mtu na kumpelekanjia isiyo sahihi ndio kule kumuua. Ni kwa muktadha huo ndio maana, kulea, kumuongoza na kumuokoa mtu mmoja kunahesabiwa kuwa sawa na kuwaokoa watu wote na kumpoteza mtu mmoja ni kama kuwaangamiza wanaadamu wote.
Njia nyingine ya kutatua shida za watu ni pale mtu anamuona Mwislamu mwenziwe akiwa katika hatari ya kutumbukia katika dhambi basi amzindue na kumnasihi na kumuusia aogope na madhara ya dhambi, au kama mtu huyo anakabiliwa na tishio la uhai na mali basi amzindue na kumbainishia hatari inayomkabili mbele yake. Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa:
"Daraja ya juu kabisa Siku ya Kiyama ni ya wale watu ambao hapa duniani wanawatakia kheri watu wengine." Kwa upande wake Imam Ali bin Abi Twalib (as) anaitambua jamii ambayo haina wa kuinasihi na wala haikubali kunasihiwa kwamba ni jamii ambayo haina kheri wala wema.
Anasema: Hakuna kheri katika watu ambao miongoni mwao hakuna wa kuwapa nasaha na si wenye kuwapenda wanaonasihi.
Kwa hakika kutoa nasaha na kumnasihi mtu kutokana na jambo baya au kumzindua mtu kutokana na hatari ya upotofu inayomkabili mbele yake, kuna umuhimu kiasi kwamba, Imam Muhammad Baqir (as) anawataja kuwa ni wafanya hiana na usaliti watu ambao wanajizuia kuwanasihi watu wengine. Anasema: "Endapo wasomi wataficha nasaha zao, basi watakuwa ni wenye kufanya khiana."
Tab'an, baadhi ya wakati ni vigumu mtu kukubali nasaha na mwongozo, kiasi kwamba, huchukia na kukasirika pale unapomkabili na kumuongoza au kumpa nasaha kuhusiana na jambo fulani baya analolifanya. Hata hivyo kuchukia na kukasirika huku kunapaswa kuvumiliwa kwani hatima yake ni nzuri.
Imam Muhammad Baqir (as) ambaye ni Imam wa Tano katika mlolongo wa Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) anasema kuwa: "Wafuate watu ambao wanakulilia wakikutakia kheri, na epukana na watu ambao wanakucheka na ambao wanakutakia mabaya.
Nukta nyingine muhimu ni hii kwamba, mwanadamu anapaswa kuwa, kwa namna ambayo awe ni mwenye kuwatakia kheri watu wengine. Kwa hakika watu ambao hawakubali nasaha na mwongozo au wanalihesabu suala la kuamrishwa mema na kukatazwa mabaya kwamba, ni kuvunjiwa heshima hujipeleka wao wenyewe katika dimbwi la hilaki na maangamizi.
Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Kukataa nasaha na kutokubali mwongozo ni chanzo cha kuangamia mwanadamu."
Nukta nyingine muhimu ni kuwa, mtoaji nasaha naye anapaswa kutumia mbinu nzuri na ya ujanja ili kumfanya yule anayemnasihi asiudhike sana, na hivyo kumuandalia mazingira ya kuipokea kwa mikono miwili nasaha na mwongozo anaompatia. Hekima na maneno mazuri ni jambo muhimu mno wakati wa kumnasihi mtu; kwani endapo mtoaji nasaha atatumia mbinu mbaya na ya maudhi au kutumia maneno ya kejeli atakuwa ameandaa mazingira ya mhusika kuikataa nasaha yake na hata wakati mwingine kuzusha tafrani baina yao. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 125 ya Surat an-Nahl: "Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema."
Kwa mfano moja ya njia za kumrekebisha mtu kutokana na aibu na mapungufu aliyonayo zilizousiwa katika dini tukufu ya Kiislamu, ni kumtajia aibu mhusika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, tena kwa heshima na upole wa hali ya juu.
Mtoaji nasaha anapaswa kutumia mbinu nzuri kiasi cha kuonekana kwamba, kazi aliyoifanya ni kama vile amempatia zawadi mhusika. Mtume (saw) amesema kuwa: Ndugu zenu bora ni wale ambao wanakuelezeni aibu zenu. Aidha anasema: Muumini ni kioo cha muumini, humuweka mbali na mabaya. Kwa hakika muumini ni kioo cha ndugu yake, akiona makosa ya muumini mwenzake inampasa, amueleze kwa uzuri na kumsaidia kurekebisha kosa hilo. Ukweli wa mambo ni kuwa, kioo huonesha aibu za mtu bila kelele na katika ukimya kamili. Kadiri kioo kitakavyokuwa kisafi basi ndivyo ambavyo aibu huonekana vizuri zaidi. Kwa maana kwamba, kadiri mtoaji nasaha anavyokuwa mtu mwema na msafi ndivyo ambavyo bila shaka nasaha na mwongozo anauotoa hupokewa kwa mikono miwili na hata kuwa na taathira zaidi.
Kuwaheshimu watu wengine kunahesabiwa kuwa aina nyingine ya kutatua matatizo ya watu. Hii ni kutokana na kuwa, akthari ya matatizo mengi ya kiroho na kisaikolojia yanayowakabili watu yanaweza kuondolewa kwa kuwakirimu na hivyo kuwafungulia njia ya uongofu. Katika Qur'ani Tukufu suala la kuwaheshimu watu wengine limezingatiwa na kupewa umuhimu maalumu. Kumheshimu mtu mwingine na kumkirimu ni jambo ambalo hukuza mapenzi baina ya watu na kuondoa hasama na mivutano isiyo na umuhimu. Aidha suala hili huimarisha mdakhala na maingiliano ya watu, jambo ambalo bila shaka huifanya jamii kutawaliwa na huba na ushirikiano. Kumheshimu na kumkirimu ndugu yako katika dini ni jambo ambalo lina ujira mkubwa katika Uislamu. Mtume (saw) anasema: Mtu ambaye anatazungumza na ndugu yake Mwislamu kwa maneno yaliyojaa huba, mapenzi na heshima na akamtatulia shida yake, basi rehema ya Mwenyezi Mungu huwa juu ya kichwa chake kama kivuli, madhali angali anafanya kazi hiyo.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki. Msisite kujiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya Faidika na Hadithi. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatu...

Comments

Popular posts from this blog

kaburi la mtume YUSHA

STAHA NA HAYA KWA MWANAMKE