TANESCO YAIPA ZANZIBAR SIKU 14
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa siku 14 kwa wadaiwa sugu wote linalowadai kulipa madeni yao, vinginevyo litawakatia huduma ya umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk Tito Mwinuka alisema shirika hilo linadai jumla ya Sh bilioni 275.38.
Alitaja makundi yanayodaiwa na shirika hilo kuwa ni wizara na taasisi za Serikali, zinazodaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) linalodaiwa zaidi ya Sh bilioni 127.87 na kampuni binafsi na wateja wadogo, ambao deni lao ni zaidi ya Sh bilioni 94.97.
“Pamoja na siku hizo 14, pia tutawapa notisi wadaiwa wote na kuwaarifu juu ya muda tuliowapa wawe wamekamilisha kulipa madeni yao, baada ya hapo shirika litachukua hatua ya kusitisha huduma ya umeme kwa wateja watakaoshindwa kuanza kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria,” alisisitiza Dk Mwinuka.
Alisema wale wateja wadogo, Tanesco haitowaandikia kutokana na sababu ya wingi wao, isipokuwa kupitia ofisi ya Uhusiano ya Shirika, wataarifiwa kupitia vyombo vya habari.
Akizungumzia malimbikizo ya madeni hayo, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema malimbikizo hayo yamekuwa yakikwamisha jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya shirika hilo kwa wakati, ikiwemo shughuli za uendeshaji shirika, matengenezo ya miundombinu na utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Alisema shirika hilo linatarajia endapo madeni hayo yatalipwa, itasaidia shirika hilo kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi zaidi, hivyo kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali, zinazotegemea nishati ya umeme nchini.
Hatua hiyo ya Tanesco, imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli, kuliagiza shirika hilo kuwakatia umeme wale wote wanaodaiwa ikiwemo taasisi nyeti za Serikali, ikiwemo Zanzibar.
Rais alitoa agizo hilo wakati akizindua ujenzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wa kilovolti 132 mkoani Mtwara, ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi.
Katika agizo lake hilo kwa Tanesco, alilitaka shirika hilo kuikatia umeme hata Ikulu, endapo haitalipa deni la umeme, ili kuliwezesha shirika hilo kujiendesha zaidi.
“Hata Ikulu kama inadaiwa wewe kata, najua pia kuna deni la Sh bilioni 162 kule Zanzibar, nako kama hawatalipa kateni umeme, tunataka Tanesco iharakishe kusambaza umeme kwa wananchi sasa wasipolipwa madeni watawezaje kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi?” Alihoji Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Nakajumo James kutoka Moshi anaripoti kuwa serikali mkoani mkoani Kilimanjaro, imeitaka Tanesco kujitathmini na kuepuka kukatika kwa umeme bila sababu za msingi, jambo linalochangia kudhoofisha ukuaji wa sekta ya viwanda.
Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema hayo baada ya kutembelea viwanda vya uzalishaji wa nondo na vifaa vingine vya ujenzi ya Five Star, Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL), Kiwanda cha Uzalishaji Maji cha Moshi Water na Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi (Moshi Technical).
“Kila kiwanda nilichotembelea malalamiko yao ya msingi ni kukatika kiholela kwa umeme huku wengine wakidai kuunguza baadhi ya vifaa vyao vya gharama kubwa, kushindwa kuzalisha kwa viwango wanavyotarajia... haya yote pia huathiri uchumi, maana hawataweza kulipa kodi,” alisema.
Awali, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Five Star, Frank Lesirian, Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Moshi Water, Jenipher Kiwia na Mkuu wa Shule ya Moshi Ufundi, Erasmus Kyara, waliomba Tanesco kuboresha huduma zake, kama sehemu ya kuunga mkono kauli mbiu ya serikali kuhusu Tanzania ya viwanda.
Akizungumzia suala la elimu, Kyara aliomba serikali kuongeza kasi ya utekelezaji mpango wake wa kukarabati shule kongwe ikiwamo yake, kwani sasa hali yake ni mbaya, jambo linaloathiri wanafunzi kitaaluma.
“Shule hii ilianzishwa miaka ya 1950 ambapo hadi kufikia sasa miundombinu yake ni chakavu mno na kama ulivyoshuhudia tunahitaji msaada...majengo yetu yamechakaa, hatuna vifaa vya kufundishia, ingawa tayari wizara imefanya tathmini na tunasubiri utekelezaji,” alisema.
Baadhi ya walimu waliomba serikali kusaidia kuweka uzio katika mabweni ya wasichana shuleni hapo kutokana na mazingira yake kuwa tata, hususani umeme unapokatika jambo ambalo linatishia usalama wao.
Comments
Post a Comment