STAHA NA HAYA KWA MWANAMKE
Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasomaji na tunakutana kwa Mara kwanza katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki cha Faidika na Hadithi. Katika kipindi hichi cha kwanza tutapenda kuwanukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na staha na haya.
Kwa kuzingatia kwamba, wanawake wanaunda nusu ya mwili wa jamii na wana nafasi muhimu katika kuleta na kueneza haya, staha, usafi na maadili katika jamii ya mwanadamu, katika kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 1 ya mfululizo
, tutajadili na kuzungumzia maudhui ya staha na haya kwa wanawake kama ilivyokuja katika hadithi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
*******
Staha na utakasifu ni jambo ambalo limechanganyika na kuumbwa mwanamke. Imam Ja’afar Swadiq (a.s) anasema kuhusiana na staha na haya kwamba: Haya ina vipengee kumi na vipengee tisa kati ya hivyo kumi vinapatikana kwa wanawake na kipengee kimoja kilichobakia kiko kwa wanaume..
Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) pia inasema: Haya ni jambo zuri, lakini kwa wanawake ni jambo zuri zaidi.
Kwa hakika hadithi hizi zinabainisha kwamba, sehemu kubwa ya masuuliya na majukumu ya kuhifadhi staha na maadili katika jamii iko mikononi mwa wanawake. Kwa kuzingatia uhakika huo, wanawake wastahiki wanapaswa kuwa makini zaidi kuliko wanaume katika kuhifadhi hijab, namna ya kuzungumza na hata katika utembeaji wao.
Tunaporejea katika Kitabu Kitukufu cha Qur’ani tunapata kwamba, suala la haya kwa wanawake limeashiriwa kwa njia mbalimbali. Katika aya ya 31 ya Surat Nur Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba, mwanamke mwenye haya na staha ni Yule anayejistiri na kuchunga heshima, staha na hijabu yake kwa mtu asiye maharimu wake.
Aya hiyo inasema:
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
Kwa msingi huo basi, ishara ya haya ni wanawake kujistiri kikamilifu na hilo ni jambo ambalo limeashiriwa katika aya iliyotangulia na wanawake wametakiwa kuiambatanisha pamoja miamala yao na kuona haya na soni. Kutoonesha uzuri wao kwa watu wasio maharimu kwao kwa wanawake waumini ni ishara na athari ya kuona haya na kuwa staha wanawake.
*******
Mtume Muhammad (saw) anabainisha na kutambulisha mavazi ya wanawake kwa wanaume ambao sio maharimu wao kwamba, ni kigezo cha ubora wa mwanamke. Anasema: Wanawake wenu walio wabora ni wanawake wenye staha, ambao hujipamba kwa ajili ya waume zao tu, na hujistiri kikamilifu kwa wasiokuwa waume zao.
Siku moja Bwana Mtume (saw) alisema: Je nikuambieni wanawake wabaya kabisa kwenu nyinyi ni wepi? Kisha akasema: Wanawake wenu walio wabaya kabisa ni wale wanaojipamba mbele ya wengine lakini mbele ya waume zao hujifunika na hawaoni ulazima wa kujipamba mbele ya waume zao.
Katika Surat al-Qasas, Qur’ani tukufu inabainisha sehemu ya maisha ya Nabii Mussa (a.s) na kisa cha kukutana kwake na mabinti wa Nabii Shuaib (a.s). Mabinti ambao mwenendo na muamala wao ulikuwa umejaa staha, haya na heshima. Kisa hicho kinaeleza kuwa, wakati Nabii Mussa (a.s) alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao mabinti wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana. Basi Nabii Mussa akawanyweshea. Baada ya mabinti wale kurejea kwa baba yao yaani Nabii Shuaib (a.s) walimhadithia kuhusiana na msaada waliopewa na bwana yule pamoja na upole na huruma aliyokuwa nayo kwao.
Nabii Shuaib (a.s) akamtuma mmoja wa mabinti zake kwa Nabii Mussa ili akamualike nyumbani. Binti Yule alikwenda mpaka alipo Nabii Mussa (a.s) na akampa habari kwamba, baba yake anamuita.
Qur’ani Tukufu inabainisha jinsi binti Yule alivyokuwa akimuendea Nabii Mussa na suala la haya, soni na staha aliyokuwa nayo kwa kusema:
Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea.
Hatua ya Qur’ani Tukufu ya kubainisha mwenendo na mabinti wa Nabii Shuaib (a.s) ni sisitizo juu ya nukta hii kwamba, kwa mtazamo wa Qur’ani, kuona haya na kuwa na staha ni miongoni mwa sifa muhimu na za ukamilifu wa mwanamke. Binti ya Nabii Shuaib sambamba na kuchunga, haya na staha alifikisha ujumbe kwa kutumia maneno machache kabisa na bila kusema maneno ya pembeni na kumjulisha Nabii Mussa juu ya wito wa baba yake na sababu ya mwaliko huo pale aliposema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea.
*******
Kwa hakika mwenendo na muamala wa wanawake na wanaume katika jamii ni jambo lenye umuhimu mkubwa mno. Kuwa na haya katika maneno na katika uzungumzaji ni jambo linalosisitizwa na Mwenyezi Mungu pale alipowahutubu wakeze Mtume (saw) pale aliposema:
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.
Pamoja na kuwa aya hiyo inawahutubu moja kwa moja wake za Mtume (saw), lakini hukumu na amri hiyo haiwahusu wakeze Mtume pekee, bali inawahusu wanawake wote wa Kiislamu. Kwa hakika haya na soni inalazimu kwamba, uzungumzaji uwe kwa namna ambayo itachochea na kumtia ushawishi mwanaume ambaye si maharimu kwa mwanamke. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mafaqihi na Marajii wa dini wanasema kuwa, kuzungumza mwanamke na mwanaume ambaye si maharimu wake, au kuzungumza mwanamke huyo kwa namna ambayo sauti yake itakuwa ni ya kuchochea hisia za matamanio za mwanaume huyo ni haramu.
Jambo jingine linalokatazwa ni mwanaume na mwanamke ambao si maharimu kufanya mzaha usio na maana. Inaelezwa kuwa, kufanya mzaha mwanaume na mwanamke ni jambo ambalo linawaweka mbali na staha na haya.
Abu Basir anasimulia kwa kusema kuwa:
Nilikuwa katika msikiti wa Kufa nikimfundisha Qur’ani mwanamke mmoja. Ghafla moja nikawa nimefanya naye mzaha na utani. Ukapita muda, kisha siku moja nikapata fursa ya kumtembelea Imam Muhammad Baqir (a.s) mjini Madina. Imam akanilaumu kwa kitendo changu kile. Niliona haya na kuinamisha kichwa changu chini. Imam Baqir (a.s) akasema: Fanya toba, na usifanye tena utani na mzaha na mwanamke ambaye si maharimu.
Bibi Fatima Zahra (a.s) ni mfano kamili wa mwanamke wa Kiislamu aliyekamilika katika kila sifa na aliyejipambana kwa kila ukamilifu. Bibi Fatima alilipa kipaumbele suala la haya na staha.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifuatacho:
Siku moja Bibi Fatima alikuwa amekaa pamoja na Bwana Mtume (saw), mara Bwana mmoja kipofu akabisha hodi na kuomba idhini ya kuingia. Mtume (saw) akamuona Fatima amesimama na kujistihi kwa hijabu. Mtume (saw) akasema, ewe binti yangu, bwana huyu ni kipofu. Bibi Fatima akamjibu baba yake kwa kumwambia: Baba yangu kipenzi, pamoja na kuwa yeye hanioni, lakini mimi ninamuona na ananusu harufu ya mwanamke. Baada ya Mtume (saw) kusikia maneno yale, akasema: Ninashuhudia kwamba, wewe ni pande la nyama yangu.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wiki ijayo.
Masha allah
ReplyDelete